Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe ameendelea kuwaweka kwenye presha watani zake Simba ambao hivi karibuni wametangaza kufanya dua maalum kwa ajili yake.
Kamwe anatamba kuwa na 'JASUSI' mitaa ya Msimbazi ambaye amekuwa akimpatia kila taarifa muhimu kutoka ndani ya uongozi wa Simba.
Kama haitoshi, jana akadokeza mpango wa Yanga kupeleka kilio Msimbazi kwa kumn'goa mmoja wa wachezaji tegemeo kwa sasa katika timu hiyo.
Kupitia chapisho lake aliloweka katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Kamwe amedokeza mchezaji huyo mkataba wake ni chini ya miezi sita hivyo kisheria Yanga inaruhusiwa kufungua nae mazungumzo na kumpa mkataba wa awali.
"Mchezaji akibakiza miezi sita kwenye Mkataba wake, sheria inamruhusu kufungua mazungumzo na klabu nyingine na kusaini Mkataba wa awali. Asante sana Injinia Hersi muda sio mrefu nitaanza kutamba na mchezaji wetu bila wasiwasi," aliandika Kamwe.
Tetesi zinazosambaa mitandaoni zinamtaja kiungo mshambuliaji Morice Abraham ambaye alijiunga na Simba katika dirisha lililopita akisaini mkataba wa mwaka mmoja.