Zikisalia siku chache kabla ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa, kuna uwezekano mkubwa kiungo wa Yanga Moussa Balla Conte akakumbana na 'Thank You'.
Licha ya usajili wake kutikisa kwenye dirisha lililopita, Conte ameshindwa kulishawishi benchi la ufundi na hata kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Wakati Yanga ikitarajiwa kuongeza nguvu eneo la kiungo cha ukabaji, nafasi ya Conte ndio inaonekana kuwa hatarini ikiwa ni kwa kutolewa kwa mkopo au makubaliano ya pande mbili.
Mkufunzi wa Yanga Pedro Gonclves akizungumza na wanahabari baada ya mchezo dhidi ya Fountain Gate ambao Wananchi walishinda kwa mabao 2-0, aliweka wazi kuwa Yanga ni timu kubwa na kila mchezaji anapaswa kupambania nafasi yake.
"Mchezaji anapopewa nafasi anapaswa kuonyesha anastahili na iwe sababu kwake kuendelea kubaki kikosini," alisema Goncalves ambaye hakufurahishwa jinsi timu yake ilicheza licha ya kuibuka na ushindi.
Goncalves anatarajiwa kuwasilisha ripoti na mapendekezo yake kwa uongozi huku Rais wa Yanga Injinia Hersi Said akiwa tayari kurudi tena kwenye dirisha la usajili kuongeza nguvu.
Conte ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni waliotua kwenye dirisha lililopita la usajili wengine wakiwa ni Mohamed Doumbia, Andy Boyeli, Celestin Ecua na Lassine Kouma.
Doumbia, Kouma na Ecua wamekuwa wakipata muda zaidi wa kucheza licha ya kuwa bado mashabiki wa Yanga hawaonekani kuridhishwa na viwango vya nyota hao wapya.