Prince Dube 'Mwana wa Mfalme' leo amewapa tabasamu mashabiki wa Yanga kwa mara nyingine akifunga bao pekee la ushindi dakika za jioooooni katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Coastal Union uliopigwa uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.
Ilikuwa mechi ngumu vijana wa Coastal Union wanaonolewa na kocha Mohamed Muya wakicheza kwa kujilinda zaidi na unaweza kusema ilibaki kidogo tu wawazuie wananchi kuondoka na alama tatu.
Ni dakika ya 87 pasi ya Pacome Zouzoua ilitua mguu kwa Duke Abuya ambaye alimimina majaro iliyotua kichwani kwa Dube aliyeandika bao muhimu la mchezo.
Kabla ya kuingia kwa bao hilo, Yanga ilipoteza nafasi kadhaa kupitia kwa Dube, Boyeli na hata Ecua ambaye mipira yake mingi iliishia mikononi mwa mlinda lango wa Coastal Union, Hassan Masalanga.
Ni alama tatu muhimu kwa Yanga ugenini ambazo zinawasogeza Wananchi hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.




