Mshambuliaji wa Yanga Prince Dube leo anatarajiwa kuwaongoza Wananchi katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi ligi ya mabingwa (CAFCL) dhidi ya JS Kabylie utakaopigwa saa 1 usiku huko Algeria.
Dube alifunga bao pekee la Yanga katika mchezo uliopita Wananchi wakiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS FAR uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Baada ya mwanzo mgumu wa msimu, Dube aliwapa tabasamu Wananchi katika mchezo ambao awali hata yeye mwenyewe hakuwa tayari kucheza kutokana na changamoto alizopitia kawenye mechi zilizopita.
Lakini wachezaji wenzake walimuamini na kumtaka avae jezi na hakuwaangusha akifunga bao lililoifanya Yanga ianze vyema hatua ya makundi nyumbani.
Bila shaka leo Dube atakuwa na nafasi nyingine ya kuendeleza pale alipoishia katika mchezo uliopita.
Wanasema mshambuliaji anapopita katika wakati mgumu huhitaji kufunga bao moja tu ili kurejesha makali yake.
Hata msimu uliopita Dube alianza kwa kuchechemea lakini baada ya kufunga bao katika mchezo dhidi ya TP Mazembe, ukawa mwanzo wa kufunga kwenye mechi mfululizo.