Klabu ya Yanga kesho Jumatano inatarajiwa kuzindua jezi rasmi ambazo zitatumika kuanzia hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika msimu huu.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amewataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuwa tayari kuzipokea jezi bora zenye kiwango cha Kimataifa.
"Kwa mujibu wa ratiba ambayo tuko nayo, mpaka sasa hivi Mwanachama wa klabu ya Yanga aandae 'kibunda' mapema jezi zinaweza kuzinduliwa siku ya Jumatano".
"Hatuna muda wa kuchelewa tunataka jezi zinunuliwe mapema watu wavae wapendeze wajiandae na safari ya kwenda New Amaan Complex," alisema Kamwe.
Yanga itaanzia nyumbani mikiki mikiki ya hatua ya makundi CAFCL ikiikaribisha AS FAR katika mchezo wa kwanza utakaopigwa Novemba 22 katika uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Msimu huu Yanga imechagua kucheza mechi zake za nyumbani ligi ya mabingwa kuanzia hatua ya makundi katika dimba la Amaan.