Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves ameanza majukumu yake kwa staili tofauti akiwaongezea wachezaji 'dozi' ya mazoezi hasa ya kuimarisha utimamu wa mwili.
Kwa nyakati tofauti msimu huu baadhi ya mashabiki wa Yanga wamesikika wakilalamika kuwa utimamu wa miili ya wachezaji uko chini na pengine ndio sababu hawalioni lile soka la kasi walilozoea kutoka kwa timu yao.
Wapo waliokwenda mbali wakiutaka uongozi kuajiri kocha mwingine wa viungo, hata hivyo Goncalves ameridhishwa na kazi inayofanywa na kocha wa mazoezi ya viungo Tshephang Mokaila alichoongeza ni aina tofauti ya mazoezi ambayo anaamini yatawafanya wachezaji wawe 'fit' zaidi.
Baada ya siku chache alizosimamia mazoezi, utofauti umeanza kuonekana huku wachezaji wakikiri mambo sio mepesi tena kama ilivyokuwa wakati wa Romain Folz aliyefutwa kazi baada ya kupoteza mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Silver Strikers.
Goncalves ameonekana akiwa na Mokaila wakipandisha utimamu wa mwili kwa mazoezi makali ya mbio za tofauti kisha baadaye kurudi kuuchezea mpira taratibu katika mazoezi hayo hayo.
Pengine mashabiki wa Yanga watarajie kuona utofauti kwa timu yao siku ya Jumapili pale watakapoikabili KMC katika uwanja wa KMC Complex
Baada ya mchezo huo, Wananchi watakuwa na wiki mbili za kujiandaa na mechi mbili za hatua ya makundi CAFCL wakianzia nyumbani dhidi ya AS FAR na kisha kusafiri Algeria kuikabili JS Kabylie.