Mchezo wa mkondo wa kwanza kuwania kufuzu hatua ya makundi ligi ya mabingwa kati ya Silver Strikers dhidi ya Yanga utapigwa Jumamosi ijayo, Oktoba 18 huko Malawi
Dakika 90 muhimu kwa Yanga ugenini kabla ya kumalizia mechi ya pili nyumbani Oktoba 25 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Licha ya utofauti wa ubora baina na Yanga na Silver Strikers, lakini ni wazi haitakuwa mechi rahisi na Yanga haitapaswa kuwadharau wapinzani wao ingawa kwenye karatasi hawapewi nafasi ya kusonga mbele
Baada ya kufanikiwa kuiondosha Elgeco Plus kwa faida ya goli la ugenini, mkufunzi wa Silver Strikers Etson-Kadenge Mwafulirwa alikiri kuwa watahitaji kuwa kwenye ubora mkubwa ili kuweza kutinga hatua ya makundi mbele ya Yanga
Kocha huyo ambaye aliiongoza Silver Strikers kupata sare ya bao 1-1 Madagascar na kisha kutoka 0-0 katika mechi ya pili dhidi ya Elgeco Plus iliyopigwa Malawi, alisema Yanga imewazidi katika ubora wa wachezaji na hata uwekezaji
Silver Strikers walitwaa taji la ligi kuu ya Malawi msimu uliopita na kupata tiketi ya kucheza ligi ya mabingwa. Msimu huu wanashika nafasi ya tatu katika ligi yao baada ya kucheza mechi 18
Katika kuonyesha Yanga imepania kutinga hatua ya makundi, kikosi kilirejea mazoezini tangu Oktoba 06 licha ya kuwakosa wachezaji 12 walioko kwenye majukumu ya timu za Taifa
Mkufunzi wa Yanga Romain Folz anaendelea na maandalizi kuwanoa vijana wake ili kuhakikisha lengo la angalau kucheza hatua ya makundi linatimia kwa msimu wa tatu mfululizo