Beki wa kati raia wa Ghana, Frank Assink, sasa anaonekana kuwa kwenye wakati wake sahihi wa kuonyesha ubora wake ndani ya kikosi cha Yanga kinachonolewa na kocha Romain Folz.
Tangu ajiunge na Yanga katika dirisha lililopita la usajili akitokea Singida BS, Assink hajapata nafasi ya kuonekana uwanjani kwenye mechi tano za mashindano ambazo timu yake imecheza.
Kufungiwa kwa beki Ibrahim Hamad ‘Bacca’ kwa mechi tano za mashindano ya ndani kumeacha nafasi wazi katika safu ya ulinzi ya Yanga. Hilo linafungua milango kwa Assink kuonyesha thamani yake na kuthibitisha kwa nini alisajiliwa Yanga.
Katika kipindi ambacho Bacca atakuwa nje, Yanga inatarajiwa kuwategemea zaidi mabeki Dickson Job na Bakari Mwamnyeto, huku Assink akiwa chaguo linalosubiriwa kwa hamu kuchukua nafasi ya Bacca.
Kwa sasa, Yanga imeanza maandalizi kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Silver Strikers. Assink ni beki wa kati pekee aliyesalia kambini baada ya Bacca, Job na Mwamnyeto wote kuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars. Hiyo ni fursa ya kipekee kwake kufanya mazoezi kwa ukaribu na benchi la ufundi.