Mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize, atakaa nje ya dimba kwa muda wa kati ya wiki tatu hadi nne kutokana na majeraha ya goti aliyoyapata hivi karibuni.
Mzize, ambaye msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara alipachika mabao 14, alipata jeraha hilo wakati Yanga ikiichapa Wiliete SC ya Angola mabao 3-0 kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Daktari wa timu ya Yanga, Moses Etutu, amesema kuna matumaini makubwa ya Mzize kurejea dimbani baada ya mapumziko ya kalenda ya FIFA.
Kuumia kwa Mzize pia kumeathiri kikosi cha Taifa Stars, ambacho kinajiandaa na mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Zambia utakaopigwa Oktoba 8 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ amelazimika kumwacha nje ya kikosi kutokana na jeraha hilo.
Msimu huu Mzize ameitumikia Yanga katika mechi mbili Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na ligi ya mabingwa dhidi ya Wiliete SC