Wakati Taifa Stars ikiendelea kupigania nafasi ya pili katika Kundi E, kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026, Kocha Mkuu wa timu hiyo ya taifa, Hemed Suleiman 'Morocco', amesema mfumo mpya wa kumtaka kila mchezaji aliye uwanjani kuwa na uwezo wa kufunga bao, ndiyo utakaoimaliza Niger leo, katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Stars itakuwa na kibarua dhidi ya timu hiyo, ukiwa ni mchezo wa saba wa Kundi E, kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia, zinazotarajiwa kuchezwa mwakani, nchini Marekani, Canada na Mexico.
Hata hivyo, matumaini pekee ya Taifa Stars sasa ni kumaliza nafasi ya pili kwani tayari Morocco imefuzu katika kundi hilo baada ya kufikisha alama 21, ikifuatiwa na Stars yenye pointi 10 na Zambia sita.
Mshindi wa kwanza katika kila kundi, atafuzu moja kwa moja huku katika makundi tisa wakitazamwa washindwa bora (best losers) watakaotinga raundi ya pili kucheza mechi za mtoano kusaka nafasi ya kwenda tena kucheza mechi za mtoano na timu kutoka mabara mengine kusaka nafasi ya kufuzu fainali hizo.
Kinachotakiwa kwa sasa ni Taifa Stars tu kupigana kushinda mechi zake mbili zilizosalia dhidi ya Niger leo na ya mwisho dhidi ya Zambia ili kumaliza na alama 16, kwani uwezekano wa kuwa mshindwa bora bado ni mdogo kutokana na pointi zilizonazo timu nyingine zinazoshika nafasi ya pili katika makundi mengine nane.
Kutoka Kundi A, Misri inaongoza ikiwa na alama 19, huku nafasi ya pili ikishikwa na Burkina Faso yenye pointi 14 ikifuatiwa na Sierra Leon na alama zake tisa huku kila timu ikibakiza mechi tatu.
Kundi B, DR Congo ipo kileleni na alama 16 ikifuatiwa na Senegal pointi 15 huku Sudan ikishika nafasi ya tatu kwa pointi 12, kila timu ikisaliwa na mechi tatu.
Kundi C, linaongozwa na Afrika Kusini yenye pointi 16, ikifuatiwa na Benin alama 11, Nigeria ikishika nafasi ya tatu na alama zake 10, kila timu ikisaliwa na mechi tatu.
Kundi D kinara ni Carpe Verde yenye alama 16, ikifuatiwa na Cameroon pointi 15 huku Libya ikiwa na pointi 11. Kundi F, Ivory Coast inaongoza kwa alama 19 ikifuatiwa na Gabon yenye pointi 18 na Burundi 10.
Kundi G, Algeria inaongoza ikiwa na alama 18, ikifuatiwa na Uganda 12 na Msumbiji 12 huku Guinea ikishika nafasi ya nne kwa alama zake 10, zote zikibakisha mechi tatu.
Kundi H, Tunisia ipo kileleni kwa alama 19, ikifuatiwa na Namibia 12 na Liberia 10 sawa na Equatorial Guinea, zote zikibakiza mechi tatu kila moja. Kundi I, Ghana ni kinara kwa alama zake 16, ikifuatiwa na Comoros pointi 15, Madagascar 13 na Mali 12, zote zikibakiza mechi tatu kila moja.
Kuelekea mchezo huo wa Stars dhidi ya Niger leo, akizungumza mjini Zanzibar jana, Morocco, alisema ametengeneza mfumo kutokana na tatizo kubwa la umaliziaji linaloikabili timu hiyo.
"Kwenye soka la kisasa makocha wamerahisisha mifumo, mchezaji yeyote anaweza kufunga, tumejaribu kufanya hivyo kwenye timu yetu, imefanya kazi kwa baadhi ya mechi za CHAN, tumeona hata mabeki wameanza kufunga, nimekuja nao huku"
"Naona kama kuna afadhali kidogo tofauti na mwanzo tulivyouanza, ukiangalia kwa sasa tunafunga ingawa japo si idadi nzuri ya mabao na hii yote ni kwa sababu tukubali ukweli kuwa tuna upungufu kwenye eneo la mbele na wenyewe mnaona jinsi gani ni ngumu kupata mshambuliaji namba tisa halisi katika nchi yetu kwa sasa," alisema Morocco.
Alisema kuwa matatizo hayo hayaanzii kwenye kikosi cha timu ya taifa bali kwenye klabu ambazo ndizo zinatoa wachezaji wa Stars.
"Ufungaji unaanzia kwenye klabu, huku timu ya taifa unawachukua tu ambao wako tayari basi unawaweka wanakufanyia kazi, lakini kama huko ni changamoto, basi hata huku ni matatizo, lakini kama nilivyosema tumelifanyia kazi kwa kutengeneza mfumo mbadala," alisema.
Stars itacheza mechi hiyo, saa 10:00 jioni, ikiwa ni siku tatu baada ya kucheza dhidi ya Congo, Ijumaa iliyopita na kutoka sare ya bao 1-1, ukipigwa, Uwanja wa Alphonce Massemba-Debat, jijini Brazaville.