Jana Yanga ilifanya Mkutano Mkuu wa Wanachama wa mwaka katika ukumbi wa Super Dome, Masaki jijini Dar es salaam ambapo mkufunzi wa timu hiyo Romain Folz akiambatana na kocha msaidizi Manu Rodriguez na Mkurugenzi wa ufundi, Paul Matthews walishuhudia Mkutano huo
Folz na wenzake katika benchi la ufundi walipata wasaa wa kushuhudia historia kubwa na mafanikio ya Yanga ambapo mataji matano waliyotwaa msimu uliopita yaliwasilishwa katika Mkutano huo


Akizungumza baada ya mkutano huo, Folz alieleza kufurahishwa na mafanikio hayo akikiri kushangazwa na sapoti kubwa ya mashabiki ambayo Yanga inayo nje ya uwanja
Amesema kwa aina ya kikosi alichonacho, anaamini wana nafasi kubwa na kuendeleza mafanikio hayo huku akiomba mwamko wa mashabiki uendelee kuwahamasisha wachezaji wake
"Nafurahi kuwa hapa, nimepata wasaa wa kuonana na kila mdau wa klabu hii, mimi, kocha msaidizi na mkurugenzi wa ufundi tumefurahi kuwa hapa"
"Tutapambana tufanye vizuri zaidi, lengo letu ni kuona tunaendeleza mafanikio haya na kufanya vizuri zaidi. Kila mechi, kila mashindano na wakati tutashuka uwanjani kupambana ili kuipa Yanga mafanikio makubwa zaidi," alisema Folz
Folz ameeleza kuridhishwa na rasilimali alizonazo kwaajili ya kuijenga timu yake huku akiwataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi Septemba 12, kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi
"Najua hii ni siku ya kipekee kwa Yanga, ni siku ya furaha na bashasha kwa wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki wetu pia, itakuwa siku nzuri kwa kila mmoja wetu," aliongeza Folz