Wakati Stephane Aziz Ki akiaga rasmi Yanga na kuelekea Wydad Athletic, mashabiki wengi walihisi pengo kubwa lingebaki kwenye kikosi cha mabingwa hao wa Tanzania.
Aziz Ki alikuwa injini ya timu akihusika kwenye mabao mengi kwa ufungaji na usaidizi jambo lililowapa hofu mashabiki kuhusu mustakabali wa safu ya kiungo.
Lakini Yanga haikupoteza muda. Ndani ya mazoezi yanayoendelea KMC Complex, jina la Mohamed Doumbia limekuwa gumzo.
Kiungo huyu mpya ameonyesha kiwango cha juu kiasi cha kumfanya aonekane kama mrithi kamili wa Aziz Ki. Wapo wanaosema Doumbia anachanganya sifa za Aziz Ki, Khalid Aucho na Clatous Chama kwa pamoja! ana maarifa, pasi makini, kasi, nguvu na uwezo wa kujituma hata bila mpira.
Hii ndiyo sababu majukwaa ya mashabiki wa Yanga yamefurika mijadala kumhusu. Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, amefanya maamuzi sahihi katika dirisha hili la usajili, kwani Doumbia na nyota wote waliotua Jangwani wameonyesha thamani yao.
Ijumaa hii, Yanga itakuwa na mechi ya kirafiki dhidi ya Rayon Sports nchini Rwanda. Mchezo huo utakuwa fursa kwa mashabiki kumshuhudia Doumbia akidhihirisha ujuzi wake uwanjani na pengine kuthibitisha kwamba moto wake wa mazoezini unaweza kuwasha pia kwenye mechi halisi.