Msimu wa 2022/23 mshambuliaji anayesubiri utambulisho Yanga Andy Boyeli aliitumikia klabu ya Power Dynamos akiibuka mfungaji bora wa ligi kuu ya Zambia akifunga mabao 18
Mafanikio yake katika msimu huo ambao pia alitwaa tuzo ya MVP, yakampa nafasi ya kutimkia Afrika Kusini kujiunga na Sekhukhune
Boyeli alisajiliwa na Dynamos akitokea klabu ya Chambishi katikati ya msimu na kufunga mabao muhimu yaliyosaidia Abayellow kutwaa taji lao la kwanza la ligi tangu mwaka 2011
Kennedy Musonda ndiye aliyekuwa nyota katika nusu ya kwanza ya msimu huo, lakini uhamisho wake kujiunga na Yanga ukampa nafasi Boyeli

Ni kama historia hiyo inajirudia tena kwani Boyeli anakuja kujiunga na Yanga kuchukua nafasi ya Musonda aliyetimkia Israel
Kabla ya kutimkia Sekhukhune, Boyeli aliweka rekodi ya kipekee ndani ya Power Dynamos, kwani idadi ya mabao yake 18 aliyofunga yalimfanya aingie katika rekodi akiwa miongoni mwa washambuliaji bora zaidi katika ligi ya Zambia kwa miaka 12 iliyopita
Mabao 18 aliyofunga katika msimu wa 2022/2023 yalimuweka katika nafasi ya tatu nyuma ya Walter Bwalya, Chris Mugalu na Idris Mbombo. Walter Binene Bwalya Sabwa alifunga mabao 24 mwaka 2016 akiwa na Nkana. Idris Mbombo na Chris Mushimba Mugalu walifunga mabao 20 mnamo 2018 na 2017, mtawalia.
Boyeli alilingana na idadi ya mabao yaliyofungwa na gwiji wa Nkana, Ronald ‘Sate-Sate’ Kampamba, mwaka 2013
Msimu wake wa kwanza Afrika Kusini katika klabu ya Sekhukhune alifunga mabao 7 katika mechi 27. Ligi ya Afrika Kusini ina ushindani na mara nyingi huwa sio ligi nyepesi kwa nyota wa kigeni. Kuna wachezaji walihitaji msimu zaidi ya mmoja kudhihirisha ubora wao