Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema klabu hiyo imewaruhusu wachezaji wake Kibwana Shomari na Denis Nkane kushiriki ‘Dar Boxing Derby’ linalotarajiwa kufanyika Julai 26, jijini Dar es Salaam.
Kamwe amesema kama klabu walipata wazo hilo kutokana na kile ambacho wachezaji hao wamekuwa wakifanya kambini wanapokuwa katika majukumu yao. Walipowashirikisha wachezaji hao, walikubali kushiriki pambano hilo
"Baada ya kupata wazo tulizungumza na wachezaji wetu wakakubali kushiriki pambano hilo kwani wanataka kuwaonyesha watanzania vipaji ambavyo hawavifahamu"
"Naamini pambano hili litaongeza thamani ya mapambano mengine yatakayofanyika siku hiyo kutokana na ubora wa wachezaji hao vile vile tunatarajia idadi ya mashabiki itazidi kuwa kubwa," alisema Kamwe
Akizungumza wakati wa kuwatambulisha wachezaji hao katika ofisi za Azam TV jana, Muandaaji wa pambano hilo Meja Selemani Semunyu amesema kuwa anaushukuru uongozi wa klabu ya Yanga kwa kuwaruhusu wachezaji hao wapande ulingoni
“Ninaushukuru uongozi wa Yanga kwa kukubali kuwaruhusu wachezaji wao kupambana siku hiyo tunaomba mashabiki wao wajitokeze kwa wingi kushuhudia burudani ya aina yake", amesema Semunyu
Wakitamba kuelekea pambano hilo, Kibwana amesema ngumi yake inaitwa katafumua, ambayo itamfanya mpinzani wake Denis Nkane ashindwe kuendelea na pambano.
“Kwa upande wangu nimejiandaa vizuri kutokana na aina ya mazoezi ninayoendelea kuyafanya kuhakikisha ninawapa burudani mashabiki wangu kutoka Morogoro,” amesema Kibwana.
Amesema hana wasi wasi kukutana na mpinzani huyo kwani anamfahamu hivyo ndani ya dakika tano ya raundi ya kwanza atakuwa amemaliza pambano.
Naye, Denis Nkane amesema Kibwana hamsumbui kwa kuwa anaamini atampa kipigo ambacho hajawahi kukutana nacho.
“Nakuja na ngumi jiwe ambayo itamfanya Kibwana asiweze kuniangalia kwani ninafanya mazoezi ambayo yatanisaidia kupata matokeo mazuri, amesema Nkane.
Yanga ni klabu inayohusisha michezo mbalimbali ( Sports Club) ikiwemo ndondi na michezo mingine