Juzi baada ya kushiriki mchezo wa hisani Kigamboni, Rais wa Yanga Injinia Hersi Said alizungumza maneno machache kwa wanahabari waliokuwa na shauku kubwa kusikia mipango ya Yanga kuelekea msimu ujao
Hersi alizungumzia mikakati ya Yanga katika ushiriki wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika msimu ujao na kidogo akagusia usajili unaofanywa na Mabingwa hao wa kihistoria
Kauli iliyowapa tabasamu mashabiki na wanachama wa Yanga ni pale aliposema katika dirisha hili Yanga inafanya usajili bora kuliko wakati mwingine wowote
Kwa maana aina ya wachezaji waliosajiliwa wana viwango vikubwa na watakwenda kuongeza uimara wa kikosi cha Yanga msimu ujao hasa katika michuano ya ligi ya mabingwa (CAF CL)
Kauli hiyo inaakisiwa aina ya tetesi ambazo Yanga imeendelea kuhusishwa nazo huku baadhi ya wachezaji wakiwa tayari wamesaini
Katika dirisha hili Yanga na Simba zimepigana vikumbo sana kwenye 'battle' za usajili. Baadhi ya sajili zilizofanywa na Yanga zinawahusu wachezaji ambao wengine walianza mazungumzo na Simba kabla ya Yanga kuingia na kuwapa mikataba
John Bosco Nchindo kiungo mshambuliaji wa klabu ya Cotton Sport ya Cameroon nae anatajwa kuwa kwenye rada za Yanga na tayari Wananchi 'wamechungulia' mahitaji ya mkataba wake uliobaki na klabu ya Cotton Sport
Huyu ni MVP wa ligi kuu ya Cameroon msimu uliopita, klabu ya Simba ilikuwa ya kwanza kuhusishwa nae
Msimu wa 2023/24 aliitumikia klabu ya Young Sports Academy katika ligi kuu ya Cameroon akifunga mabao 13 na asisti 4 kabla ya kutimkia Cotton Sport msimu uliopita ambapo katika mechi 16, alifunga mabao 7 na kutoa asisti 2
Ni mchezaji mwenye umri wa miaka 23 ambaye ana kipaji na pia nafasi ya kuendea kuwa bora zaidi
Inaelezwa bado Yanga inatafuta kiungo mshambuliaji mwingine kuziba nafasi iliyoachwa viungo Stephane Aziz Ki na Clatous Chama
Licha ya taarifa za ndani kudokeza klabu kuwa na makubaliano binafsi na Feisal Salum ili arejee Jangwani, Azam Fc wameweka ngumu kumuachia kirahisi wakihitaji angalau Bil 1.3
Fei Toto bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Azam Fc, Yanga haiko tayari kutoa kiasi hicho majadiliano yakiwa yanaendelea baada ya kuwasilisha ofa rasmi kwa matajiri hao wa Chamazi
Hivyo endapo mpango wa kumrejesha Fei Toto utakwama, pengine Mcameroon John Bosco Nchindo anaweza kuchukua nafasi