Klabu ya Yanga SC imeweka bayana dhamira yake ya kuhakikisha inashinda mechi zote tatu zilizobaki katika Ligi Kuu ya NBC ili kutetea ubingwa wake kwa mara ya nne mfululizo na kufikisha jumla ya mataji 31 ya ligi hiyo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema kuwa malengo ya timu hiyo ni makubwa, na kwamba kila mchezo uliobaki ni fainali kwao.
"Niwaombe wananchi tuwe pamoja katika mechi hizi tatu ili kuhakikisha tunakwenda kutetea ubingwa wetu kwa mara ya nne," alisema Kamwe.
Yanga inakabiliwa na michezo mitatu ya mwisho ambayo Kamwe ameitaja kuwa ni ya "maamuzi" dhidi ya Tanzania Prisons, Dodoma Jiji, na Simba SC.
Mchezo wa kwanza katika orodha hiyo ni dhidi ya Tanzania Prisons, utakaopigwa Jumatano ya Juni 18 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya. Kamwe amesema timu itasafiri kutoka Dar es Salaam ikiwa na lengo moja tu, kubeba alama tatu muhimu.
"Mchezo unaofuata ni dhidi ya Tanzania Prisons, tunakwenda Mbeya tukiwa na lengo moja tu, kuchukua alama tatu mbele ya Prisons," alieleza Kamwe huku akihimiza mashabiki kujitokeza kwa wingi.
Kwa mujibu wa Kamwe, maandalizi ya msafara wa mabasi kuelekea Mbeya yanaendelea, huku akitoa wito kwa Wanayanga wa Mbeya na mikoa ya jirani nao kufika kwa wingi kuisapoti timu.
Baada ya mechi dhidi ya Prisons, Yanga itaelekea Zanzibar kwa pambano la pili dhidi ya Dodoma Jiji FC litakalochezwa Juni 22 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.
Msimu wa ligi utahitimishwa kwa mtanange wa watani wa jadi, Yanga dhidi ya Simba SC, utakaopigwa Juni 25 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, mchezo ambao huenda ukawa wa kuamua bingwa wa msimu huu.
Yanga inakwenda katika mechi hizo ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na alama 73. Ushindi katika mechi utawahakikishia Wananchi kuhifadhi taji lao kwa msimu wa nne