Wakati bodi ya ligi ikiendelea kusisitiza mchezo namba 184 wa ligi kuu ya NBC kati ya Yanga dhidi ya Simba uliopangwa kupigwa Juni 15 kuwa upo, klabu ya Yanga ambayo ni mwenyeji wa mchezo huo imebainisha kuwa mchezo huo haumo katika ratiba yao na hivyo hakuna maandalizi yoyote yanayofanyika upande wao
Hivi karibuni Msemaji wa Bodi ya ligi Karim Boimanda wakati akihojiwa na Azam Tv, alisema maandalizi ya mchezo huo yanaendelea vyema na karibuni watatangaza utaratibu wa uuzwaji tiketi za mchezo huo
Meneja wa Habarii na Mawasiliano wa Yanga amesema kwa mujibu wa kanuni timu mwenyeji ndio yenye jukumu la kutangaza utaratibu wa mauzo ya tiketi kwani ni wao walioingia makubaliano na N-Card sio Bodi ya ligi wala mtu mwingine yeyote
"Kwa mujibu wa kanuni sisi wenyeji wa mchezo ndio tunahusika na maandalizi muhimu ikiwa ni pamoja na kutangaza viingilio vya mchezo husika. Sisi tuna makubaliano na N-Card juu ya uuzwaji wa tiketi. Baada ya mchezo uliopaswa kupigwa March 08 kutofanyika, tuliwaambia N-Card wasitishe mauzo ya tiketi"
"Hivyo watu pekee ambao wanapaswa kutangaza uuzwaji wa tiketi ni sisi na hata N-Card watahitaji ruhusa yetu ili kuuza tiketi"
"Sisi hatujatangaza kuuza tiketi na tumesema hakuna tiketi zitauzwa tena kwa Wananchi kwa ajili ya mchezo wa Juni 15 kwani msimamo wetu hatutacheza," alisema Kamwe