Ligi Kuu ya NBC imeingia kwenye hali ya sintofahamu kufuatia taarifa ya timu tano kutishia kugomea mechi mbili za mwisho za msimu huu.
Timu hizo zimeweka msimamo kuwa hazitashiriki mechi hizo hadi pale Bodi ya Ligi (TPLB) itakapotoa majibu ya kueleweka kuhusu malalamiko ya uendeshaji wa waamuzi na ukiukwaji wa kanuni kwenye michezo ya hivi karibuni.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo makini, timu hizo tayari zimewasilisha barua rasmi kwa bodi hiyo, zikielezea kutoridhishwa kwao na kile wanachokieleza kuwa ni mfululizo wa matukio ya upendeleo wa waziwazi na ukiukwaji wa kanuni za mchezo bila hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Klabu ya Yanga SC ni miongoni mwa timu hizo, ikiwa tayari ipo kwenye mgogoro na TPLB. Klabu hiyo imeshatangaza msimamo wake wa kutocheza mechi dhidi ya watani wao wa jadi Simba SC iliyopangwa kuchezwa Juni 15, na sasa huenda pia ikasusia mechi zake mbili za mwisho za ligi.
Hatua hii ya klabu hizo, iwapo itatekelezwa, inaweza kusababisha mpasuko mkubwa ndani ya ligi na kuathiri mustakabali wa msimu mzima. Aidha, huenda ikaleta athari kwa uaminifu wa mashabiki, wadhamini, na taswira ya soka la Tanzania kwa ujumla.