Methali ya Kiswahili isemayo mbio za sakafuni huishia ukingoni inaakisi vyema hali halisi ya msimu wa soka Tanzania kwa klabu ya Simba SC. Katika msimu ambao mashabiki wake walijawa na matumaini makubwa, hatima ya furaha yao sasa ipo mikononi mwa wapinzani wao wa jadi β Young Africans SC (Yanga).
Katika Ligi Kuu ya NBC, Yanga ipo kileleni kwa alama 73 baada ya mechi 27, na wakibakisha michezo miwili tu, ushindi kwenye michezo yote unatosha kuwatangazia ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo. Hili linaiondolea Simba nafasi yoyote ya kutwaa taji hilo β taji ambalo mwanzoni mwa msimu walilitamani sana.
Mechi namba 184 dhidi ya Simba iliyokuwa ipigwe Machi 8, iliahirishwa kwa mazingira tata baada ya Simba kutofika uwanjani. Hatma ya mechi hiyo haijulikani kwani Yanga imeweka ngumu kucheza hadi Bodi ya Ligi itakapofuata utaratibu halali.
Licha ya maelekezo ya CAS, Yanga imepeleka malalamiko BMT (Baraza la Michezo la Taifa), kwa kuwa TFF ni miongoni mwa waliolalamikiwa, jambo linaloonyesha msimamo wa Wananchi 'kukomaa' kutafuta haki ambayo wanaamini wanastahili.
Matumaini mengine ya Simba ya kubeba taji msimu huu yamebaki kwenye Kombe la CRDB. Hata hivyo, safari hiyo si nyepesi. Wanatakiwa kuwatoa Singida Black Stars katika nusu fainali, kisha kukutana na Yanga fainali β kama Wananchi watabaki na kasi waliyonayo, basi Simba watakutana na kizingiti kingine cha maumivu mikononi mwa mahasimu wao.
Kilicho wazi ni kuwa Yanga haitakubali kuwa ngazi kwa watani zao hao na itapambana kuhakikisha inabeba mataji yaliyobaki na hivyo kushinda mataji yote ya ndani msimu huu.Β
Kabatini tayari Yanga ina Ngao ya Jamii na kombe la Muungano walilotwaa mapema mwezi huu visiwani Zanzibar michuano ambayo watani zao Simba walijitoa wakiweka nguvu katika kombe la Shirikisho (CAF CC) ambalo wamelikosa
Kwa hali ilivyo sasa, ni sahihi kusema Yanga inashikilia furaha ya watani zao hao. Ikiwa Yanga watafanikiwa katika mechi zao zilizobaki na kuchukua tena kombe la CRDB, basi historia itaandikwa kuwa msimu wa 2024/25 Yanga ilibeba makombe yote ya ndani huku watani zao wakitoka patupu