Klabu ya Yanga SC inaendelea kuandika historia kwenye soka la Tanzania ikiweka dhamira ya kulinyakua tena kombe la CRDB Cup kwa mara ya nne mfululizo
Kesho Jumanne, Aprili 15, miamba hiyo ya Jangwani itashuka dimbani kwenye Uwanja wa KMC Complex kuwakabili Stand United katika mchezo wa robo fainali wa michuano hiyo ya Shirikisho
Yanga ambao ni mabingwa watetezi, wameonyesha ubabe mkubwa kwa kutwaa taji hilo kwa misimu mitatu mfululizo. Safari yao ya kutawala CRDB Cup haijawa ya bahati nasibu bali ni matokeo ya mipango thabiti, kikosi imara na ari ya ushindi isiyoyumba
Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Yanga imeweka rekodi ya aina yake kwa kushinda mechi 21 mfululizo kwenye michuano hii – rekodi inayozidi kuonesha ukubwa wa klabu hiyo na namna ilivyojikita katika mafanikio ya kudumu
Kocha wa Yanga, Milodu Hamdi na benchi lake la ufundi, wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kuchukulia kila mechi kama fainali. Wamesisitiza kuwa licha ya historia nzuri ya timu yao, hawaichukulii mechi dhidi ya Stand United kwa wepesi, wakijua wazi kuwa wapinzani wao nao wanahitaji mafanikio
Mashabiki wa Yanga kote nchini wanaimani timu yao itaendeleza ubabe kwenye CRDB Cup na watafuzu nusu fainali mbele ya Stand United
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amewataka Wananchi kujitokeza kwa wingi KMC Complex kuipa hamasa timu yao inayowania tiketi ya kufuzu nusu fainali
Aidha baada ya watani zao Simba kufuzu nusu fainali jana, Yanga itahitaji kusonga mbele kwani ipo nafasi ya kukutana na watani zao hao ambao waliingia mitini katika mchezo wa ligi kuu