Mikiki mikiki ya ligi kuu ya NBC inaendelea leo ambapo mchezo mmoja unatarajiwa kupigwa jijini Dar es salaam
Mabingwa watetezi wa ligi hiyo Yanga wanaendelea na kampeni ya kuhifadhi taji lao kwa msimu wa nne mfululizo pale wakiwakaribisha Coastal Union katika mchezo utakaopigwa uwanja wa KMC Complex
Hii itakuwa mechi ya mzunguuko wa 25, maana yake baada ya mechi ya leo, zitasalia mechi tano tu kuhitimisha msimu
Benchi la ufundi la Yanga limeweka wazi, linauchukulia mchezo huu kwa umuhimu mkubwa wakihitaji alama zote tatu ili kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi
Yanga iko kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama nne, ushindi utawafanya waongeze gap dhidi ya watani zao Simba wakati huo pia wakisubiri hatma ya kesi waliyofungua CAS wakizihitaji alama tatu za mchezo dhidi ya Simba uliopaswa kupigwa March 08
Meneja wa Yanga Walter Harrison amesema wanaelekea katika mchezo huo wakiwa na kikosi kamili, hakuna majeruhi wachezaji wote wakishiriki maandalizi ya mwisho hapo jana
Unatarajiwa kuwa mchezo mgumu, Coastal Union hawajawahi kuwa wepesi mbele ya Yanga
Yanga imetangaza mchezo huu ni 'Mashati Day' ikiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi huku wakiwa katika mavazi yao ya mashati...!