Kocha Mkuu wa Yanga Miloud Hamdi amesema hakuna nafasi ya kufanya makosa katika mechi zilizosalia kwani dhamira yake ni kuona Yanga inatetea ubingwa wa ligi kuu ya NBC ambao wanaushikilia kwa misimu mitatu mfululizo
Kesho Jumatatu, April 7 Yanga itakuwa mwenyeji wa Coastal Union katika mchezo utakaopigwa uwanja wa KMC Complex
Akizungumza katika Mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo, Hamdi amesema ili kuweza kutwaa taji la ligi kuu, ni lazima washinde kila mechi kwani matokeo hayo yatawahakikishia kukusanya alama nyingi kuliko timu nyingine
Amesema wachezaji ni lazima watambue umuhimu wa mchezo dhidi ya Coastal Union na kuhakikisha wanapata ushindi
"Tumejiandaa vizuri kuelekea mchezo wetu wa kesho dhidi ya Coastal Union. Tulikuwa na mchezo mzuri dhidi ya Tabora United na tunaamini tutakuwa na mchezo mzuri kesho tena dhidi ya Coastal Union, maana mchezo wa kesho hautakuwa mchezo rahisi na tunakwenda kucheza kwa umakini ili kuhakikisha tunaondoka na alama 3 muhimu"
"Nimeongea na wachezaji, nimewaelekeza watazame mchezo huu kuwa ni muhimu kwetu kwa sababu licha ya kufanya vizuri bado tuna mbio za ubingwa"
"Ili kuweza kutimiza malengo yetu, tunapaswa kupata matokeo mazuri katika mchezo huu na mingine itakayofuata," alisema