Baada ya kukosa mchezo wa kirafiki dhidi ya Singida Black Stars kutokana na matatizo ya kifamilia, nahodha wa Yanga Bakari Nondo Mwamnyeto amerejea kikosini katika maandalizi ya mchezo wa hatua ya 16 bora kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Songea United utakaopigwa kesho Jumamosi March 29 katika uwanja wa KMC Complex
Meneja wa Yanga Walter Harrison alisema Mwamnyeto alipewa ruhusa kushughulikia masuala ya kifamilia na ndio sababu hakuwa sehemu ya wachezaji waliosafiri mkoani Singida katika uzinduzi wa uwanja wa Singida Black Stars lakini tayari amerejea kuendelea na majukumu yake
Aidha Walter amesema wachezaji ambao walikuwa katika majukumu ya timu za Taifa wanatarajiwa kujiunga na wenzao kuanzia leo
Yanga ilitoa wachezaji 10 kutumikia timu zao za Taifa katika mechi za kuwania kufuzu kombe la Dunia 2026
Wachezaji hao ni Dickson Job, Ibrahim Bacca, Mudathir Yahya na Clement Mzize (Tanzania)
Wengine ni Khalid Aucho (Uganda), Duke Abuya (Kenya), Prince Dube (Zimbabwe), Djigui Diarra (Mali), Kennedy Musonda na Clatous Chama (Zambia)