Rais wa Yanga Injinia Hersi Said akiongozana na Mtendaji Mkuu Andre Mtine na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga wamekutana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh Palamagamba Kabudi katika Mkutano alioitisha kusaka suluhu ya mchezo namba 184 ligi kuu ya NBC kati ya Yanga dhidi ya Simba uliopaswa kupigwa March 08 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Akizungumza katika mkutano na wanahabari muda mfupi baada ya kutoka katika kikao hicho, Injinia Hersi amesema wamewasilisha ujumbe wao kwa Waziri ambao ni msimamo wao kama timu
"Tumekutana na Waziri Mh Palamagamba Kabudi na Mkutano huu ulikuwa muhsusi kujua nini klabu ya Yanga inakiendea, majadliano ya mchezo namba 184 dhidi ya Simba uliopangwa kuchezwa March 08, 2025"
"Uongozi wa Yanga ukiwa umeambatana na Wajumbe wote wa Kamati ya utendaji pamoja na Mtendaji Mkuu, uliweza kukutana na Mh Waziri, Mh Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa ajili ya kujadili kitu ambacho kilitokea"
"Bahati nzuri klabu ya Yanga imepata nafasi ya kuwakilisha yale ambayo ni ya msingi kabisa kuhusiana na mchezo ule, lengo la Waziri na jopo lake walitaka kusikia ujumbe wetu na sisi tukiwa kama viongozi tunasimamia maslahi ya taasisi yetu kwa niaba ya Wanachama na timu kwa ujumla"
"Kwa hiyo tuliwasilisha ujumbe unaohusiana na msimamo wetu kama Taasisi. Mh Waziri na timu yake wakatusikiliza kwa kirefu na wakapata nafasi ya kuuliza maswali kutaka kujua na tuliweza kufikisha ujumbe vizuri"
"Mh Waziri alikuwa na mwanzo mzuri na kueleza kwamba jukwaa hilo haliwezi kufanya maamuzi isipokuwa analitumia ili kuweza kupata ufumbuzi wa kile kilichotokea kwa hiyo alitaka kujifunza kutoka kwa Yanga juu ya nini hasa kinachowasibu na upi msimamo wao"
"Tumeweza kufikisha yote ambayo tunastahili kuyafikisha kama viongozi ambayo yanabeba ujumbe wa Kamati ya Utendaji lakini pia ni ujumbe wa Wanachama wetu, wapenzi na mashabiki wetu nchi nzima"
"Ujumbe huo umefika Mh Waziri na timu yake wameupokea na tumewaachia waufanyie kazi na tumekubaliana tutakuwa na vikao vingine endelevu kwa ajili ya kutafuta mwafaka wa jambo hili"
"Nichukue fursa hii kuwaambia Wanachama na Mashabiki wa Yanga sisi tuko hapa kwa ajili ya kusimamia maslahi ya taasisi yetu, niwatoe hofu sisi viongozi wao ni viongozi imara na tuko hapa kwa ajili ya kusimamia maslahi ya timu yetu. Wakae kwa kutulia, tutawajulisha mwafaka ambao utafikiwa," alisema Hersi