Jioni ya leo katika uwanja wa KMC Complex, Yanga itaanza kampeni ya kutetea kombe la Shirikisho la CRDB kwa kumenyana na Copco Fc ya Mwanza katika mchezo wa raundi ya pili (64 bora)
Hii itakuwa mechi ya kwanza kwa Yanga baada ya kuhitimisha kampeni ya ligi ya mabingwa hatua ya makundi wiki iliyopita
Kocha Mkuu wa Yanga Sead Ramovic amesema anauchukulia mchezo huu kwa uzito mkubwa na anachohitaji ni kuona vijana wake wanashinda ili kusonga mbele raundi ya tatu
Romovic amesisitiza malengo makubwa ya Yanga ni kutetea taji la CRDB kwa msimu mwingine
Katika mchezo huo huenda mabadiliko yakashuhudiwa katika kikosi cha Yanga wachezaji ambao hawapati nafasi mara kwa mara wakitarajiwa kuanza
Aidha inaweza kuwa nafasi kwa mashabiki wa Yanga kuwashuhudia nyota wapya waliosajiliwa katika dirisha dogo
Katika karatasi ni mechi ambayo ushindi unaonekana wazi upande wa Yanga hata hivyo wachezaji wa Yanga hawapaswi kuwadharau wapinzani wao hao ambao wanashiriki ligi daraja la kwanza