Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema kila Wananchi ameumizwa na matokeo ya mchezo dhidi ya MC Alger jana ambayo yameinyima Yanga nafasi ya kufuzu robo fainali ligi ya mabingwa
Hata hivyo wanapaswa kusahau matokeo hayo na kuweka nguvu katika kumaliza vyema msimu kwa kutetea mataji yao yote
Kamwe amesema huzuni ambayo mashabiki wa Yanga wameipata wanapaswa kuigeuza kuwa hamasa ambayo itawaongezea morali katika kuhakikisha wanatetea mataji yote
"Tunawashuru Wanachama na Mashabiki wote mliokuja jana Uwanja wa Mkapa. Uwepo wenu na Sauti zenu zilikuwa na thamani sana"
"Ya jana yameshapita na yatupasa kusahau. Kila Huzuni tuliyonayo moyoni, tuigeuze kuwa hamasa ya kutupa morali ya kuupambania ubingwa wetu wa LIGI KUU na KOMBE LA CRDB"
"Tuko katikati ya mapambano na yatupasa kujidhatiti kweli kweli kurudisha makombe yetu kabatini. Hili ni muhimu kuliko vyote tusongeni mbele kama kauli mbiu inavyosema," alisema Kamwe
Mwanzoni mwa Februari Yanga itarejea rasmi katika kampeni ya kutetea ubingwa wa ligi kuu kwa mchezo dhidi ya Kagera Sugar
Kabla ya mchezo huo, Yanga itamenyana na Gapco katika mchezo wa raundi ya tatu kombe la Shirikisho la CRDB