Kocha Mkuu wa Yanga Sead Ramovic amesema wamejiandaa kwa mechi nyingine ngumu ya ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons dimba la KMC Complex hapo kesho
Baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mashujaa Fc, mabingwa hao watetezi wanarudi tena KMC Complex kusaka alama nyingine tatu ambazo zinaweza kuwasogeza juu zaidi katika msimamo wa ligi
Akizungumza katika Mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo, Ramovic amesema anafahamu Tanzania Prisons ni miongoni mwa timu ngumu kufungika kutokana na umahiri wao katika kujilinda
Hata hivyo amesema wamejiandaa kimbinu kuhakikisha wanatengeneza nafasi nyingi katika mchezo huo ili kupata ushindi
"Tunatambua kuwa tuna mchezo mgumu siku ya Kesho, Wapinzani wetu ni Wazuri na bila shaka watakuja na mfumo wa kuzuia zaidi, Sisi tunajiandaa vizuri kuhakikisha tunatengeneza nafasi nyingi ili kupata Ushindi"
"Sote tunauheshimu mchezo wa Soka, Kesho hatutaangalia Historia za mechi zetu zilizopita dhidi Tanzania Prisons, Jukumu letu kesho ni kuweka Jitihada Asilimia 100% ili kupata Alama tatu tu," alisema Ramovic
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, mlinda laango Aboutwalib Mshery amewaalika mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi katika mchezo huo huku akiahidi watapambana ili kushinda
"Kwetu sisi maandalizi yetu ni mazuri na kesho tutakwenda kucheza kutokana na Maelekezo ya Mwalimu ambayo tayari ametupatia na Leo tunakwenda kufanya maandalizi ya Mwisho, Jambo kubwa na la Muhimu ni kwamba tunahitaji Kuwaona Wanachama, Wapenzi na Mashabiki wa Yanga Uwanjani ili kutusapoti, Sisi tunaahidi Ushindi," alisema