Jana katika mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya TP Mazembe, Kocha Mkuu wa Sead Ramovic alianza kipindi cha kwanza kwa kujihami zaidi
Ramovic alifahamu Mazembe ambao walikuwa nyumbani, wangeingia katika mchezo huo wakiwa na uhitaji wa bao la mapema na walianza mchezo huo kwa kasi
Yanga haikutengeneza nafasi za maana katika kipindi cha kwanza, ni nafasi moja tu ya wazi ambayo ilitengenezwa na Pacome Zouzoua lakini Kennedy Musonda alishindwa kuitumia
Baada ya Yanga kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao 1-0, Ramovic hakuwa na sababu ya kuendelea na mfumo alioingia nao katika kipindi cha kwanza
Ndipo akawaingiza Clement Mzize na Stephane Aziz Ki akiwatoa Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya ambao unaweza kusema 'mechi iliwakataa'
Kuingia nyota hao na baadae Clatous Chama kulibadili taswira ya mchezo Mzize akiwa na athari chanya zaidi
Kipindi cha kwanza Mazembe walikuwa wakitumia upande wa kulia (upande wa Kibabage) kupeleka mashambulizi yao lakini alipoingia Mzize alifanya kazi nzuri ya kurudi nyuma kumsaidia Kibabage na kusukuma mashambulizi haraka mbele pale alipopata mpira
Mzize alifanya majaribio mawili muhimu moja likienda nje na moja likasababisha bao la Yanga baada ya shuti lake kutemwa na mlnda lango wa Mazembe kabla ya Dube kumalizia
Mzize kwa sasa amejipambanua kuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Yanga, kurejea kwake ni habari njema kwa Wananchi ambao watakuwa na dakika 270 ngumu za kuamua nafasi yao ya kucheza robo fainali ya ligi ya mabingwa msimu huu