Kikosi cha Yanga kesho kitashuka dimba la July 05, 1962 kumenyana na MC Alger katika moja ya mechi mbili muhimu za ugenini katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Baada ya kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya Al Hilal, Wananchi wanahitaji kupambana kwelikweli kuhakikisha mechi ya kesho hawapotezi ili kuweka hai matumaini ya kufuzu robo fainali
Wakitoka Algeria,Wananchi wanakabiliwa na mechi nyingine ugenini ambapo kikosi kitasafiri DR Congo kuikabili TP Mazembe katika mechi itakayopigwa Disemba 14
Ili kujiweka katika nafasi nzuri Yanga inahitaji kukusanya angalau alama nne ugenini na kushinda mechi mbili zitakazokuwa zimebaki nyumbani
Maana yake ni kuwa malengo hayo yanapaswa kuanza kutimia kesho pale katika dimba la July 05 katika mchezo ambao mazingira yake yanaweza kuinufaisha Yanga
MC Alger hawatakuwa na sapoti ya mashabiki wao baada ya kufungiwa na CAF kutokana na vurugu walizofanya katika hatua ya kuwania kutinga makundi
Mara mbili ambazo Yanga ilikwenda kucheza Algeria kabla, ilikumbana na mazingira yasiyo rafiki nje ya uwanja lakini wakati huu kuna utofauti mkubwa
Kocha Mkuu wa Yanga Sead Ramovic amekiandaa kikosi chake kwa lengo la kusaka ushindi ugenini licha ya kukiri mchezo huo hautakuwa mwepesi
Habari njema kwa Yanga ni kuingia katika mchezo huo ikiwa na kikosi chenye wachezaji wengi ambao wana uzoefu wa kushiriki mashindano hayo ya CAF katika misimu mitatu iliyopita
Idadi kubwa ya wachezaji walikuwepo wakati Yanga inacheza fainali ya kombe la Shirikisho (CAF CC) na pia walikuwepo wakati Yanga ikicheza robo fainali ya ligi ya mabingwa msimu uliopita