Wakati tetesi zikisambaa huko mitandaoni kuhusu kiungo Pacome Zouzoua, ukweli ni kuwa Yanga haina mpango wa kuachana na nyota wake muhimu
Pacome, Yao Kouassi na Khalid Aucho ni miongoni mwa wachezaji ambao wako katika mwaka wa mwisho wa mikataba yao na uongozi wa Yanga umedhamiria kuwapa mikataba mipya
Walifanya hivyo msimu uliopita kwa kuwaongeza mikataba wachezaji kama Djigui Diarra, Stephane Aziz Ki, nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto na hata Clement Mzize ambaye Wydad walikuwa tyari kumng'oa Jangwani kwa kitita cha Tsh Bilioni 1
Baada ya Yanga kumsajili Clatous Chama, ni kama Simba wanatafuta mwanya wa kupoza machungu ya kuporwa mchezaji wao muhimu
Lakini kwa Yanga hii ya GSM, haitakuwa rahisi mchezaji anayehitajika kuondoka kwani Wananchi wana malengo makubwa ya kutawala soka la Afrika
Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi ameweka wazi msimamo wake ili kufikia mafanikio makubwa katika soka la Afrika hupaswi kuuza wachezaji wako muhimu
"Tuna Maono mapana tukihitaji kuwa moja ya vilabu vikubwa afrika hivyo hakuna namna tunaweza kuwaruhusu kuondoka wachezaji wanaotegemewa kuifikisha timu mbali," alisema Gamondi katika moja ya mahojiano yake wakati Mzize akihusishwa na Wydad