Akiwa katika msimu wake wa nne ndani ya Yanga, kiungo Khalid Aucho amesema hafikirii kuondoka katika kikosi cha mabingwa hao wa Tanzania Bara kwa misimu mitatu mfululizo
Nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Uganda ameendelea kuwa nguzo muhimu katika safu ya kiungo cha Wananchi, mkataba wake ukimalizika mwishoni mwa msimu
Akizungumza na waandishi wa habari jana Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere muda mfupi kabla ya kikosi cha Yanga kupaa Arusha, Aucho alisema mkataba wake kumalizika isitafsiriwe kama anaondoka kwani anaamini atafikia makubaliano na mabosi wake ili asalie
"Nani amewaambia kuwa naondoka Yanga? nimesema huu ni msimu wa mwisho kwenye mkataba wangu, sijasema ni mwisho wangu wa kucheza Yanga"
"Suala la mkataba mpya liko kwenye mazungumzo, hivyo tusubiri," alisema Aucho
Yanga inatarajiwa kumuongeza Aucho mkataba baada ya kuanza nae mazungumzo huku kukiwa na taarifa kuwa dirisha dogo Yanga itasajili kiungo mwingine mkabaji ili kuongeza nguvu katika eneo hilo
Baada ya kukosa mchezo uliopita wa ligi dhidi ya JKT Tanzania akitumikia adhabu ya kadi tatu za njano, Aucho anatarajiwa kurejea uwanjani kesho Jumamosi kuikabili Coastal Union katika mchezo utakaopigwa dimba la Sheikh Amri Abeid