Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya JKT Tanzania ambao utapigwa kesho Jumanne katika uwanja wa Azam Complex
Akizungumza katika Mkutano na wanahabari mapema leo, Gamondi alisema anatambua JKT Tanzania ni timu ngumu msimu huu lakini watakwenda kukabiliana nao wakiwa na lengo moja tu, kusaka ushindi
Gamondi amesisitiza mchezo huo ni mpya, matokeo ya mabao 5-0 waliyopata msimu uliopita hayana nafasi. Anachohitaji ni vijana wake kushinda pasipo kujali idadi ya mabao
"Tupo tayari tena kujianda na mchezo mwingine. Tunakwenda kucheza na timu ambayo imepoteza mchezo mmoja na kutoka sare michezo minne"
"Kimsingi wanaonekana ni wagumu lakini tunajua nini chakufanya. Nafahamu msimu uliopita tulishinda magoli matano, walikuwa na timu tofauti na mwalimu tofauti"
"Kwangu mimi sitazami yaliyopita. Yaliyopita yamepita natazama yajayo, nimewaona wanavyocheza msimu huu wapo vizuri hivyo nakwenda kucheza nao kwa namna wanavyocheza na sio kutazama awali walikuwaje"
"Naomba niweke sawa jambo hili kwa mashabiki, mimi mipango yangu sio timu ifunge magoli mengi, mimi napenda timu yangu itengeneze magoli mengi. Yakipatikana magoli mengi sawa lakini lengo kuu ni alama tatu," alisema Gamondi