Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema anatambua mchezo wa ligi kuu dhidi ya Pamba Jiji hpo kesho hautakuwa mwepesi lakini wamejipanga kushinda
Akizungumza katika mkutano na Wanahabari, Gamondi amesema Pamba wamekuwa na mwanzo usioridhisha wa msimu wakikosa ushindi katika mechi sita
Amesema ni kawaida kila timu inapocheza na Yanga, wachezaji wanahamasika zaidi na kufanya mechi kuwa ngumu
"Tumecheza mechi nne mfululizo, sio ratiba rafiki sana ya wachezaji kujiandaa na kuwa na utimamu kamili wa kimwili. Lakini tupo tayari kwa mchezo wa kesho. Hata hivyo tunajua tutakumbana na mchezo mgumu. Kimsingi haitupi shida sana kwani tumejipanga kiakili na kimwili tupo imara"
"Nimewafuatilia Pamba, wanacheza vizuri kitimu, wanazuia kutokea chini na kufanya mashambulizi kwa kushitukiza. Nafahamu wamefunga magoli mawili na kuruhusu mabao matano"
"Hautakuwa mchezo mwepesi kwetu hasa tukizingatia kila timu inayocheza nasi wachezaji wanahamasika zaidi lakini tumejipanga kushinda," alisema Gamondi
Katika hatua nyingine Gamondi amesema anaridhishwa kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake katika mechi zilizopita
Gamondi amesema sio tatizo inapotokea mchezaji anacheza chini ya kiwango katika baadhi ya mechi, kwani nao ni binadamu
"Wakati mwingine kuna changamoto ya uchovu. Mfano tulipokwenda kucheza Ethiopia baadhi ya wachezaji walitoka katika majukumu ya timu za Taifa hivyo baadhi yao walikuwa na changamoto kubwa ya uchovu"
"Aziz Ki na Khalid Aucho wamekuwa bora kwangu, hawawezi kucheza katika ubora ule ule katika kila mechi. Binafsi sioni kama wachezaji hawa wameshuka viwango kwa sababu wanatimiza majukumu yao kama ninavyowaelekeza," alisema