Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema ushindi wa bao 1-0 waliopata Ethiopia dhidi ya CBE SA ni matokeo muhimu kwao kuelekea mchezo wa mkondo wa pili utakaopigwa Jumamosi, Septemba 21 katika uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar
Hata hivyo Gamondi ameonyesha kutofurahishwa na vijana wake kutotumia nafasi nyingi walizotengeneza katika mchezo huo
Akizungumza jana muda mfupi baada ya kikosi kutua kutoka Ethiopia, Gamondi alisema alitarajia mchezo ungekuwa mgumu lakini pia kama wangekuwa makini mechi hiyo wangeimaliza hukohuko Ethiopia
"Nilitarajia haitakuwa mechi nyepesi kwetu, changamoto ya hali ya hewa na hata uwanja haukuwa katika hali nzuri ya kucheza mpira wa miguu"
"Msisahau tulikuwa na wachezaji 14 ambao walikuwa kwenye majukumu ya timu za Taifa, tukiungana nao siku mbili kabla ya mechi"
"Lakini pamoja na yote, nikiri tulistahili kumaliza mechi hii Ethiopia kwani tulitengeneza nafasi nyingi ambazo tulishindwa kuzitumia. Sifahamu kwa nini tulikosa nafasi vile"
"Tumerejea nyumbani, tutakuwa na siku chache za kujiandaa na mechi ya marudiano. Tunahitaji kushinda ili tusonge mbele hatua ya makundi," alisema Gamondi
New Amaan Complex ndipo mechi ya mkondo wa pili itachezwa, CAF wakitoa ruksa kwa Yanga kutumia uwanja huo