Licha ya kikosi chake kuonyesha ubora mkubwa katika mechi za mwanzo msimu huu, Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema haimaanishi kama wako salama na itakuwa rahisi kwao kupata mafanikio kama ilivyokuwa msimu uliopita
Gamondi amesema msimu huu anatarajia kupata upinzani mkali zaidi kutoka kwa wapinzani wao katika michuano yote wanayoshiriki kwani kila timu inajiandaa kwa lengo la kushindana na Yanga
Gamondi maefichua kuwa kila mara amewataka wachezaji wake wapambane zaidi kwani timu zote zimejiandaa kutaka kuwafunga
"Kila timu sasa inataka kuifunga Yanga, inabidi tupambane, tusijidangaye kuwa tupo kwenye mstari salama, ninawaambia haya hata wachezaji wangu, wanatakiwa kila siku waongeze juhudi na mazoezi zaidi ili tuwe bora kila kukicha kwani wenzetu nao wanaongeza ubora ili watufikie au watupite"
"Na si kwenye soka tu, hata kwenye maisha ni lazima uwe na presha ya kusaka maisha, kuweza kulipa kodi, kutunza nyumba, kulisha watoto, kuwalipia ada, yote hii ni presha na hiyo ndiyo inakufanya uwe makini na ujitume," alisema Gamondi
Katika msimu huu, Yanga imeweka malengo ya kutetea taji la ligi kuu kwa msimu wa nne mfululizo, kutetea taji la FA kwa msimu wa nne ikiwa tayari imerejesha Ngao ya Jamii waliyokuwa wameipoteza kwa Simba msimu uliopita
Baada ya kufika robo fainali ya ligi ya mabingwa msimu uliopita, Yanga imelenga kuvuka hatua hiyo msimu huu ambapo kwanza Wananchi wanahitaji kutinga hatua ya makundi
Mechi ya kwanza ya kusaka tiketi ya makundi itapigwa Jumamosi ya wiki hii huko Ethiopia dhidi ya CBE SA na marudiano kupigwa jijini Dar es salaam wiki moja baadae