Kocha wa zamani wa Yanga Nasreddine Nabi hivi karibuni alikuwa nchini kwa ajili ya masuala yake binafsi ambapo pia alipata nafasi ya kufika Makao Makuu ya Yanga, Jangwani na akafanya mazungumzo na viongozi waandamizi wa klabu hiyo
Taarifa zaidi zimebainisha kuwa Nabi aliwasilisha ofa kutoka klabu ya Kaizer Chiefs kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji ambaye kwa sasa ndio habari hapa nchini, Clement Mzize
Hata hivyo katika mahojiano yake, kocha huyo raia wa Tunisia hakuwa tayari kufichua ya ndani yaliyomleta kuzungumza na GSM na viongozi wa Yanga lakini alisema amefurahi kurudi tena nchini huku akiwapongeza vongozi wa Yanga kwa kuunda kikosi imara ambacho anaamini msimu huu kitafanya makubwa katika michuano ya ligi ya mabingwa
"Nimekutana na viongozi wa Yanga tumekuwa na vikao vizuri vya kifamilia, nilifanya kazi hapa, bado nina maelewano mazuri na viongozi lakini pia wachezaji hata mashabiki na wanachama," alisema Nabi na kuongeza:
"Nimefurahia kuona kila ninapopita bado watu wanakumbuka kuhusu Nabi, watu wa Yanga, Simba na hata timu nyingine, nimewaambia viongozi kuwa wana timu nzuri sana msimu huu, sitashangaa kama watavuka mbali zaidi ya hatua ya makundi kwa kucheza robo fainali na hata nusu fainali"
"Nadhani ni timu chache zinaweza kuwa na kikosi kizito kama hiki cha Yanga, naamini watafanya vizuri sana hapa ndani na hata Afrika", alisema Nabi
Nabi amepewa jukumu la kuisuka upya Kaizer Chiefs ambayo kwa misimu kadhaa imepoteza nguvu yake katika soka la Afrika Kusini na Afrika kwa jumla
Wakati wa pre-season Yanga ilialikwa na Kaizer Chiefs kushiriki Tamasha la Toyota Super Cup Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 4-0