Aliyekuwa mshambuliaji wa Azam Fc Prince Dube amesema ndoto ya kila mshambuliaji ni kucheza timu moja na viungo ambao watamrahisishia kazi ya kufunga mabao
Dube jana alikuwa mkoani Morogoro ambako alishiriki Tamasha la Wape Tabasamu akifanikiwa kufunga moja ya mabao ya timu Job iliyoshinda mabao 6-2 dhidi ya timu Kibwana
Katika moja ya maswali ambayo aliulizwa na wanahabari kabla ya mchezo huo, ni hili la kuhusishwa na Yanga ambayo pia inahusishwa na kiungo Clatous Chama na wakati huohuo ikiwa imefanikiwa kumbakisha mfungaji bora wa ligi kuu msimu uliopita, Stephane Aziz Ki
Dube amesema yuko nchini kushiriki Tamasha hilo, kuwaunga mkono wachezaji wenzake lakini itakuwa furaha kwake kama atacheza na Chama na Aziz Ki katika timu moja
"Litakuwa jambo la furaha sana, Aziz Ki na Chama ni wachezaji wazuri ambao kila mchezaji angependa kuwa nao katika timu moja. Hivyo kama itakuwa hivyo nitafurahi sana," alisema Dube
Chama na Aziz Ki walitajwa kuwa wangeshiriki Tamasha hilo lakini haikuwezekana kwa kuwa kila mmoja alikuwa na majukumu kama hayo katika nchi zao
Lakini kinachozungumzwa huenda wachezaji hao (Aziz Ki, Chama na Dube) wote wakaitumikia Yanga msimu ujao
Hivi karibuni Aziz Ki alifichua kuwa msimu ujao hana mpango wa kuwania tuzo ya mfungaji bora kwa sababu atakuwa na jukumu la kumtengenezea nafasi Dube aweze kushinda tuzo hiyo
"Mimi siwezi kuwa mfungaji bora msimu ujao. Dube anakuja hapa hivyo kazi yangu itakuwa kumtengenezea nafasi yeye na Guede (Joseph) ili washinde tuzo hiyo," alisema Aziz Ki