Dodoma Jiji leo wameingia kwenye mfumo wa Wananchi, almanusra mnara wa 5G usome! likibaki bao moja tu Yanga ikishinda mabao 4-0 katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Jamhuri
Licha ya kuwa tayari ni mabingwa, Yanga yenye mabadiliko ya wachezaji nane walioanza katika mchezo dhidi ya Ihefu Fc, ilihitaji dakika 9 tu kuanidika bao la kuongoza kupitia kwa Clemet Mzize aliyemalizia krosi ya Joyce Lomalisa
Stephane Aziz Ki alikuwa jambo lake leo, akafunga bao la pili dakika za majeruhi kipindi cha kwanza baada ya yeye mwenyewe kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari
Aziz Ki akafunga bao la tatu dakika ya 51 likiwa la pili kwake katika mchezo huo akimalizia pasi ya Mzize
Yanga iliendelea kutawala kipindi cha pili na lilikuwa suala la itafunga mabao mangapi
Msumari wa nne ulipigiliwa na Maxi Nzengeli katika dakika ya 78 baada ya Yanga kufanya shambulizi la kushitukiza
Aziz Ki angeweza kuondoka na mpira siku ya leo, Dodoma Jiji watapaswa kumshukuru mlinda lango wao Aron Kalambo ambaye aliokoa michoyo kadhaa ya Aziz Ki
Aziz Ki sasa amerejea kwenye usukani katika mbio za kuwania ufungaji bora akifikisha mabao 17