Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe amewataka Wanachama na Mashabiki kuhakikisha wanajisajili na kulipa ada zao za uanachama ili kuipa klabu nguvu kubwa ya kiuchumi na hatimaye kuweza kuwabakisha wachezaji wote muhimu na kuendelea kufurahia mafanikio
Kamwe amesema amepokea simu na ujumbe mwingi kutoka kwa mashabiki ambao wanaulizia kuhusu hatma ya kiungo Stephane Aziz Ki ambaye mkataba wake unamalizika siku chache zijazo pale msimu utakapofika tamati
Kamwe amesema lengo la Yanga kuhakikisha wachezaji wote muhimu wanaendelea kuitumikia timu hiyo msimu ujao lakini haitawezekana kama hakutakuwa na fedha za kutosha
"Mashabiki wengi wananipigia simu kuhusu Aziz Ki. Sasa niwaambie kama wewe ni shabiki wa Yanga na hulipi kadi ya uanachama basi ujue wataondoka wachezaji wengi tu"
"Ili Aziz Ki abaki lazima klabu iwe na hela na hela zinatoka kwetu sisi. Tumewapa fursa ya kulipa ada kupitia matawi ya NBC. Je wachezaji wanabaki vipi ikiwa wewe hulipi ada?," alihoji Kamwe
Uongozi wa Yanga unapambana kumbakisha Aziz Ki lakini kuna upinzani mkali kutokana na mchezaji huyo kupata ofa nono zaidi kutoka kwa timu nyingine
Klabu za Mamelodi Sundowns, Kaizer Chiefs zote kutoka Afrika Kusini zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili Aziz Ki huku Al Ahly nao wakiwa tayari kumn'goa Aziz mikononi mwa Wananchi