Baada ya kuipa Yanga taji la tatu mfululizo la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema uongozi imara ndani ya klabu hiyo ndio chachu kuu ya mafanikio yao
RJuzi ikiwa ugenini Yanga ilitangaza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar na kufikisha pointi 71 ambazo hazitafikiwa na timu nyingine yoyote zikiwa zimebakia mechi tatu kumaliza msimu
Gamondi amesema uongozi wa Yanga ulioko chini ya Rais Hersi Said, umekuwa imara na unafanya mambo makubwa katika kikosi hali iliyopelekea kupata matokeo mazuri msimu huu na kutangaza ubingwa kabla ya msimu haujamalizika
Kocha huyo raia wa Argentina alisema klabu kubwa ya soka inahitaji uongozi imara ili kusimamia na kufanikisha malengo yao na hilo limetokea kwa Yanga ambapo uongozi umekuwa karibu na timu na kuhakikisha mambo yote muhimu yanapatikana
"Ubingwa huu sio tu wachezaji wameufanikisha, lakini pia nitoe pongezi kwa uongozi wa klabu yetu, wamekuwa karibu na timu, wamekuwa wakiendesha mambo kisasa zaidi na kufanikisha mafanikio haya," alisema Gamondi
Gamondi alisema wachezaji wake wameonyesha ukomavu mkubwa na kufuata misingi imara iliyowafikisha katika mafanikio. Alisema wachezaji wote wa Yanga wamekuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja pamoja na kujituma muda wote wanapokuwa uwanjani kwa ajili ya kusaka ushindi jambo lililowafikisha walipo sasa
"Nidhamu, kujituma na kupambana muda wote uwanjani kwa wachezaji wangu hii pia ni sababu ya mafanikio haya, wachezaji wangu kila mmoja amefanya kazi yake vizuri, kila mchezaji anapopata nafasi anapambana kuipa ushindi timu, huwezi kuacha kuwasifia wachezaji"
Aidha Gamondi amebainisha kuwa hakupata shida katika suala la nidhamu ya wachezaji, kila mmoja alifanya kazi yake vizuri kujituma kila alipopata nafasi yakucheza. Pia kocha huyo alisema kikosi kipana chenye wachezaji wenye ubora walichonacho kimechangia kutwaa ubingwa wa msimu huu
Gamondi alisema hata pale aliopokuwa akiwakosa baadhi ya wachezaji, waliopewa nafasi walikuwa wakionyesha kiwango kizuri na kutoonyesha utofauti
"Viongozi walikuwa makini kwenye usajili, nimekuwa na wachezaji ambao uwezo wao ni mkubwa, kila aliyepata nafasi alionyesha kitu, kuwa na kikosi kipana kulinipa wigo wa kuchagua wachezaji wa kucheza kulingana na aina ya mechi," alisema Gamondi
Gamondi hakuwaacha mashabiki wa klabu hiyo akibainisha kuwa ni sehemu ya mafanikio kwa sababu walionyesha upendo kwa timu yao na kuwaunga mkono katika kila mchezo kitu kilichoongeza hamasa kwa wachezaji
"Shabiki ni mchezaji wa 12, unapocheza mbele ya mashabiki na wakawaunga mkono kinaongeza kitu kwenye timu, tumekutana na hali hii kutoka kwa mashabiki wa Yanga, wamefanya kazi yao na niweke wazi wamechangia ubingwa huu," alisema Gamondi