Leo Yanga itakuwa uwanja wa Azam Complex kuikaribisha Kagera Sugar katika mchezo wa ligi kuu ya NBC raundi ya 26
Huu utakuwa mchezo wa pili baina ya timu hizo kukutana msimu huu baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Kaitaba kumalizika kwa matokeo ya suluhu ya bila kufungana
Katika msimu huu Kagera Sugar ndio timu pekee ambayo bado haijachezea kichapo kutoka kwa Yanga kwenye ligi, timu nyingine zote zimekumbana na kipigo cha Wananchi. Baadhi ya timu zikiongozwa na Simba , zimeichangia Yanga alama sita
Utakuwa mchezo mgumu kwani kila timu itaingia katika mchezo huo ikiwa na malengo tofauti
Yanga imepania kufunga hesabu za ubingwa mapema hivyo inahitaji kushinda leo ili kukaribia ubingwa wa 30
Kagera Sugar wako nafasi ya 7 wakiwa na alama 30 kama watashinda watafikisha alama 33 na kupanda mpaka nafasi ya tano na hivyo kuwa katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya nne ili kupata tiketi ya kucheza kombe la Shirikisho msimu ujao
Aidha Fred Felix Minziro Kocha wa Kagera Sugar anafahamika kwa kutengeza timu ngumu kupitika kirahisi leo anakwenda kukabiliana na timu iliyofunga mabao mengi zaidi katika ligi kuu ya NBC msimu huu
Yanga imepachika mabao 56 katika mechi 25 huku ikiruhusu mabao 12, ndio timu yenye uwiano mkubwa wa mabao kuliko timu nyingine zote
Stephane Aziz Ki leo atahitaji kufunga angalau bao moja kuifikia rekodi ya mabao 16 iliyowekwa na Fiston Mayele katika misimu miwili iliyopita
Ushindani kati yake na Feisal Salum katika mbio za kuwania ufungaji bora utakuwa chachu kwa Aziz Ki kuhakikisha leo anajiongezea idadi yake ya mabao
Mchezo utapigwa kuanzia saa 1 usiku..