Mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize amesema kiu yake ni kufunga bao katika mechi ya Jumamosi dhidi ya Simba
Mzize ambaye katika mechi ya Jumapili iliyopita alitoa pasi mbili za mabao, Yanga ikishinda mabao 3-0 dhidi ya Singida Fountain Gate, Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, alisema baada ya kutoa 'asisti' mbili katika mechi hiyo, sasa anatamani kutupia katika mechi ya 'dabi', itakayochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi
Straika huyo anaamini kuwa mchezaji anapofunga katika mechi ya 'dabi' basi rekodi inaendelea kubaki na kukumbukwa kwenye historia ya soka la Tanzania, pamoja na rekodi za michezo hiyo ya watani
"Nimetumwa na wachezaji wenzangu, wameniambia niwaambie mashabiki wajae kwa wingi uwanjani ili tuwafurahishe, tusipowaona wao mioyo yetu inafifia, lakini tukiona wamejaa na wanatushangilia na sisi tunakuwa na morali ya hali ya juu sana"
"Naamini katika mechi ya Jumamosi tutapata ushindi, nakumbuka katika mechi dhidi ya Simba iliyopita 'niliasisti' mara mbili, sasa kwenye mechi hii naweza kufunga kabisa, natamani iwe hivyo ili kuzidi kuwafurahisha wanachama na mashabiki wa Yanga," alisema Mzize
Mzize amekuwa katika kiwango bora katika mechi mbili zilizopita ambazo Yanga walicheza na Dodoma Jiji (FA) na mechi ya ligi dhidi ya Singida Fountain Gate
Kocha Miguel Gamondi ameonyesha kuwa na imani kubwa kwake hata katika zile nyakati ambazo anakumbana na ukosoaji kutoka kwa mashabiki kwa kukosa nafasi nyingi za wazi
Baada ya mechi dhidi ya Mamelodi Sundowns, Mzize anaonekana kurejea kivingine ambapo katika mechi mbili zilizopita amefunga bao moja na kutoa assist mbili