Licha ya kuumizwa na dhurma ambayo Yanga walifanyiwa huko Afrika Kusini katika mchezo wa mkondo wa pili robo fainali ligi ya mabingwa dhidi ya Mamelodi Sundowns, Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amewapongeza wachezaji wake kwa kujitoa na kupambana kwa dakika zote 180 za mchezo dhidi ya Mamelodi Sundowns
Gamondi amesema kwa jinsi wachezaji walivyojituma dhidi ya timu inayotajwa kuwa bora zaidi barani Afrika kwa sasa, walistahili zaidi ya kile walichopata
Gamondi amemwagia sifa kiungo Jonas Mkude kwa kuonyesha kiwango bora katika mechi zote mbili, akiingia kikosini baada ya Khalid Aucho kukosekana
Katika mechi hizo Mkude alidhihirisha bado anaweza kucheza mechi yoyote ya ushindani katika kiwango cha juu
"Kama kuna pongezi za kwanza naweza kuzitoa basi ni kwa wachezaji wangu wote hizi mechi mbili wamecheza kwa kiwango cha juu sana, watu wasisahau tumecheza dhidi ya Mamelodi yenye kila rekodi na kila kitu"
"Tulikuwa na changamoto za kutokamilika kwa wachezaji wetu baadhi lakini ni kama hakukuwa na hilo pengo kila mchezaji amecheza kwa kiwango kikubwa sana na kuitetea klabu kama familia"
"Mkude alifanya kazi kubwa katika eneo la kiungo, tunahitaji kuwa na wachezaji wanaothubutu kufanya makubwa kama hivi kila mmoja akipewa nafasi, natarajia Sasa ataendelea na muendelezo kama huu huko mbele zaidi," alisema Gamondi
Mkude alitua Yanga akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na Simba msimu uliopita
Alisaini mkataba wa mwaka mmoja lakini ni wazi Yanga inaweza kumuongeza mkataba mwingine kama hasa kama ataendeleza ubora alioonyesha katika mechi dhidi ya Sundowns