Kazi imefanyika vyema uwanja wa Benjamin Mkapa Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Medeama katika mchezo wa raundi ya nne ligi ya mabingwa barani Afrika
Ulikuwa mchezo wa upande mmoja kwa muda mwingi pengine Yanga ilistahili kufunga mabao zaidi ya matatu
Alikuwa ni Pacome Zouzoua aliyetangulia kufunga bao la uongozi kwenye dakika ya 33 akipiga shuti nje kidogo ya 18
Yanga ilikuwa na uwezo wa kumaliza mchezo huo kwenye kipindi cha kwanza Stephane Aziz Ki, Maxi Nzengeli na Kennedy Musonda wakikosa nafasi adimu
Yanga ilikwenda mapumziko ikiwa na uongozi wa bao 1-0. Kipindi cha pili ikarejea na kasi waliyomaliza nayo kusaka mabao zaidi
Mapema katika kipindi cha pili Medeama wakapata mkwaju wa penati baada ya Mwamnyeto kufanya madhambi ndani ya eneo la hatari pongezi anastahili Djigui Diarra aliyeokoa mkwaju huo
Mpira wa kichwa wa Kennedy Musonda ambao ulimgonga Mwamnyeto ukajaa kambani kuifungia Yanga bao la pili kwenye dakika ya 61 kabla ya Mudathir Yahya kuongeza bao la tatu kwenye dakika ya 66 baada ya walinzi wa Medeama kufanya makosa katika eneo lao
Ni ushindi ambao unairejesha Yanga katika mbio za kuwania nafasi ya kutinga robo fainali baada ya kufikisha alama 5 na kupanda mpaka nafasi ya pili ikiwa sawa na Al Ahly




