Saa 11 jioni ya leo Jumamosi, August 26 2023 Yanga itashuka uwanja wa Azam Complex, kuikabili Asas Fc katika mchezo wa mkondo wa pili hatua ya awali ligi ya mabingwa barani Afrika
Ni Maxi Day, hii ikiwa siku maalum kwa Wananchi kuingia dimba la Azam Complex kuishangilia timu yao huku wakiwa wamechomekea kama afanyavyo kiungo wao mahiri Max Mpia Nzengeli
Yanga ikiwa mbele kwa mabao 2-0 ushindi waliopata kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wakiwa ugenini, ushindi siku ya leo au hata matokeo ya sare yatawapeleka raundi ya kwanza ambako watachuana na El Merrikh ya Sudan
Kutokana na ubora wa kikosi cha Kocha Miguel Gamondi matarajio ya mashabiki wa Yanga ni timu yao kuibuka na ushindi mnono
Katika Mkutano na Wanahabari jana, Gamondi alisema mchezo wa leo unatarajiwa kuwa tofauti na mchezo wa kwanza
Gamondi alisema anatarajia Asas Fc watakuja kwa nguvu zaidi lakini amewaambia wachezaji wake hawapaswi kuwadharau
"Hatupaswi kuwadharau wapinzani wetu, mchezo huu tunaanza upya, matokeo yakiwa 0-0 dhamira yetu ni kushinda ili tusonge mbele," alisema
Kila la kheri Wananchi, kila la kheri mabingwa wa Tanzania...!