Pamoja na kuwa amewaaga rasmi Wananchi kuwa hataendelea kuwa kocha wa timu yao, Nasreddine Nabi ataendelea kubaki katika mioyo ya mashabiki wa Yanga
Ule ukame wa mataji Nabi aliumaliza kibabe kwa kushinda mataji sita katika misimu miwili pamoja na kucheza fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika
Pamoja na kikosi chake kuwa na wachezaji bora kutoka nje ya nchi, Nabi alifanya kazi kubwa ya kuimarisha viwango vya wachezaji wa ndani
Takribani wachezaji wazawa saba mpaka nane walikuwa na uhakika wa kucheza kwenye kikosi chake cha kwanza katika mechi za ligi na hata Kimataifa
Nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Kibwana Shomari, Salum Abubakar, Mudathir Yahya, Farid Mussa na hata Clement Mzize hawa ni wachezaji ambao walikuwa na uhakika wa kucheza wakipishana katika baadhi ya mechi
Nyota hawa wazawa ilifikia wakati wakatishia uhakika wa kupata nafasi kwa nyota wa kigeni
Mfano baada ya Nabi kumuamini Bacca katika nafasi ya ulinzi wa kati, Job akahamia upande wa safu ya ulinzi ya kulia, akampa wakati mgumu Djuma Shabani
Kibwana akamnyima nafasi Joyce Lomalisa ambaye kumekuwa na taarifa kuwa ameomba kuondoka, Mudathir akamnyima uhakika wa kucheza kila mechi mchezaji bora wa ligi kuu 2021/22 Yannick Bangala huku Sureboy akipishana na Stephane Aziz Ki
Nabi aliwaamini wachezaji wazawa, imani ambayo walilipa kwa kufanya vizuri kila walipopewa nafasi ya kucheza