Yanga ilianza michakato ya mabadiliko miaka ya 90

Shabiki NambaMoja By Shabiki NambaMoja
β€’
8 Mar 2018
Yanga ilianza michakato ya mabadiliko miaka ya 90
Jina la Tarimba Abbas, Mkurugezi wa kampuni ya Sportpesa Tanzania sio geni masikioni mwa Watanzania hususani mashabiki na wapenzi wa soka wa klabu ya Yanga.

Tarimba aliwahi kuhudumu nafasi mbalimbali za uongozi katika klabu ya Yanga kuanzia mwaka 1993.

Ni miongoni mwa viongozi wa kwanza kabisa waliojaribu kufanya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu ya Yanga, kutoka utegemezi wa wafadhili na kwenda kwenye kampuni.

Yanga imekuwa ikijaribu kufanya mabadiliko mara kwa mara bila mafanikio.

Fuatilia mahojiano yaliyowahi kufanywa kati ya Tarimba na Sport Kitaa kutaka kujua nini kiliikwamisha Yanga kushindwa kufanya mabadiliko miaka hiyo.

Ikumbukwe Yanga ya sasa chini ya Katibu Mkuu wake Charles Mkwasa imeuanzisha tena mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji.

Swali: Hebu tueleze, nini kilikusukuma hadi kuingia Yanga

Tarimba: Baada ya kuwa shabiki na mwanachama wa kawaida kwa kipindi kirefu, ndipo mwaka 1993 niliamua kujitosa kwenye uchaguzi wa klabu.

Nilichaguliwa kuwa Katibu Mipango wa klabu. Kazi kubwa ya mtu wa nafasi hii ni kupanga na kushauri uongozi na klabu nini cha kufanya ili maisha yaendelee klabuni.

Swali: Ulikumbana na magumu yapi katika nafasi hiyo?

Tarimba: Haikuwa kazi rahisi kwangu kumudu nafasi hiyo kutokana na mazingira niliyokutana nayo, pamoja na umri wangu, tulihitaji muda wa kujifunza zaidi.

Kama unavyojua kuwa Yanga ina utamaduni na mila zake kama vile kusoma visomo. Ilinichukua muda kidogo kuelewa, lakini hatimaye nilikubaliana nazo kwa sababu Yanga ni klabu ya wananchi wa kawaida ambayo inatoa nafasi kwa kila mmoja.

Swali: Kati ya hayo magumu unayosema, yapi unayakumbuka?

Tarimba: Changamoto kubwa ambayo nilikumbana nayo mwanzoni ni kubadilisha mtazamo wa klabu hiyo kutoka kujiendesha kiridhaa na kufuata misingi sahihi ya kampuni.

Tulipoingia madarakani, taratibu Yanga ikaanza kujibadilisha na zama za ufadhili ndipo zikaingia na wafadhili wa mwanzoni kabisa walikuwa Abbas Gulamali (marehemu), alikuwepo Murtaza Dewji na Mohammed Virani.

Hawa wafadhili walikuwa wanatoa fedha zao kwa mapenzi tu na ufadhili wao haukuwa wa kimikataba hata kidogo.

Swali: Ufadhili wao ulikuwa na mipaka ipi?

Tarimba: Hawa wafadhili hao hawakuwa na mipaka ya ufadhili, walitumia pesa na muda wao mwingi kuihudumia Yanga popote.

Swali: Ni kwa vipi mlilisimamia vuguvugu la mabadiliko?

Tarimba: Kimsingi kulikuwa na hitaji la mabadiliko katika usimamizi na uendeshaji wa klabu na kutokana na hali halisi iliyokuwa ikiikabili klabu, kulikuwa na mgogoro baina ya klabu na wafadhili, aliyekuwa Katibu Mkuu, George Mpondela Γ’β‚¬ΛœCastroÒ€ℒ ndipo akaja na wazo la mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu.

Mpondela alileta wazo la kampuni baada ya wafadhili kujiondoa. Kwa bahati mbaya alishindwa kuliendesha wazo lake kutokana na migogoro.

Tulilipokea wazo na tukaona tutengeneze mfumo wa klabu kujiendesha lengo ni kuachana na wafadhili waliokuwa wakituyumbisha.

Swali: Mlifanikiwa kwa kiasi gani katika hili?

Tarimba: Tulifanikiwa kwa kiasi kikubwa na ninakumbuka mara ya kwanza, Yanga ilipata udhamini wa kwanza wa kisasa kutoka Kampuni ya Mobitel (sasa Tigo), ambao ulifanya timu ianze kulipa mishahara kwa wachezaji na kiwango cha kwanza cha mshahara kilikuwa Sh50,000.

Tulikwenda kwenye matawi yote, kwa ajili ya kuwaelimisha wanachama mabadiliko na kuwapa nafasi ya kuuliza maswali ili waweze kukifahamu kile ambacho tunakilenga.

Hapo ndipo ulipoibuka mgogoro wa Yanga Asili na Yanga Kampuni, kwamba Kampuni walikubali na Asili hawakutaka mabadiliko chini ya Yusuf Mzimba.

Swali: Nini hasa kilikuwa chanzo cha mgogoro?

Tarimba: Chanzo kikubwa ni mgongano wa kimaslahi kwa baadhi ya watu ndani ya klabu, ni tamaa tu ya watu wachache ambao waliamini iwapo mabadiliko yatafanyika, hawatapata nafasi ya kupata masilahi binafsi ndani ya klabu hiyo, hilo liko wazi.

Swali: Sasa nini kilifanyika baada ya mgogoro kuibuka?

Tarimba: Mimi nilikuwa muumini wa mabadiliko, mgogoro ulikuwa mkubwa sana, Yanga Asili ndiyo ilikuwa chini ya uenyekiti wa Mzimba. Kundi hili lilikuwa kubwa na mgogoro ukashika hatamu, tukashindwa kufanya mabadiliko hayo tuliyoyatarajia
ADVERTISE HERE

Yanga SC Stories

Maandalizi ya kuikabili Mashujaa Fc yamekamilika
Maandalizi ya kuikabili Mashujaa Fc yamekamilika
3h ago
READ MORE β†’
Aziz Ki amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
Aziz Ki amemaliza adhabu, tayari kurejea kikosini
8h ago
READ MORE β†’
Tunajua tumewaumiza, tuko tayari kupambana - Dladla
Tunajua tumewaumiza, tuko tayari kupambana - Dladla
12h ago
READ MORE β†’
Yanga mpya kuanza na Mashujaa Fc, hivi hapa viingilio
Yanga mpya kuanza na Mashujaa Fc, hivi hapa viingilio
13h ago
READ MORE β†’
Hersi akimpata huyu wamekwisha!
Hersi akimpata huyu wamekwisha!
13h ago
READ MORE β†’
Droo ya makundi CAF ni Jumatano
Droo ya makundi CAF ni Jumatano
14h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumatatu, Oktoba 26 2026
Magazeti ya leo Jumatatu, Oktoba 26 2026
18h ago
READ MORE β†’
Yanga yarejea Dar, kujipanga dhidi ya Mashujaa Fc
Yanga yarejea Dar, kujipanga dhidi ya Mashujaa Fc
1d ago
READ MORE β†’
Behlulovic anasubiri simu ya Injinia Hersi
Behlulovic anasubiri simu ya Injinia Hersi
1d ago
READ MORE β†’
Yanga yaondoka Arusha, kituo kinachofuata ni Mashujaa Fc
Yanga yaondoka Arusha, kituo kinachofuata ni Mashujaa Fc
1d ago
READ MORE β†’