Moja ya changamoto ambayo imekuwa ikiitesa Yanga katika mechi za Kimataifa ni kutotumia vyema uwanja wa Benjamin Mkapa
Hili ni jambo ambalo kila shabiki wa Yanga analifahamu na ndio maana misimu michache nyuma Yanga iliomba kutumia uwanja wa CCM Kirumba katika mchezo wa mtoano kombe la Shirikisho dhidi ya Pyramids
Msimu huu katika mechi za CAF ukiondoa mechi ya awali dhidi ya Zalan Fc, Wananchi walilazimishwa sare dhidi ya Al Hilal (1-1) na suluhu dhidi ya Club Africain (0-0)
Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe amekiri matokeo hayo yanawaumiza sana lakini safari hii wachezaji wameahidi kuwapa furaha mashabiki wao katika mchezo dhidi ya TP Mazembe
Kamwe amesema kwa maandalizi wanayofanya, ukiongeza ari na morali ya wachezaji wanayo nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo
"Ni kweli, sote tunafahamu hatukuwa na matokeo mzuri kwenye uwanja wa nyumbani kimataifa. Tumewapa jukumu Wachezaji kuleta ushindi, tumeongea nao na wametuahidi wataipigania nembo ya klabu siku ya Jumapili kuhakikisha tunashinda," alisema Kamwe
Aidha Kamwe amesema wanajivunia uwepo wa nyota sita kutoka DR Congo ambao wamecheza mechi kadhaa dhidi ya TP Mazembe akiamini wachezaji hao watakuwa na msaada mkubwa katika mchezo wa Jumapili
"Wachezaji waliotoka Congo wanamsaada mkubwa kuikabili Tp Mazembe kwa kuwa Wachezaji wote (6) Djuma, Lomalisa, Mayele, Bangala, Kisinda na Moloko wameshacheza dabi dhidi ya Mazembe, tunaamini watakuwa na mchango mkubwa"