Mshambuliaji wa Yanga Fiston Mayele leo anatarajiwa kuwaongoza Wananchi katika mchezo muhimu wa kombe la Shirikisho dhidi ya Club Africain ambao utapigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Yanga inahitaji kushinda mchezo huo utakaopigwa saa kumi jioni ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya makundi
Mayele ndiye kinara wa mabao katika michuano ya CAF hatua za mtoano akifunga mabao saba
Jana alipokuwa akizungumza na wanahabari, kocha mkuu wa Club Africain Bertrand Marchand alikiri kumfahamu Mayele na alijaribu kumsajili katika klabu aliyokuwa akiifundisha awali kabla ya kujiunga na Club Africain
Kocha huyo pia aliwataja Jesus Moloko na Tuisila Kisinda kuwa wachezaji anaowafahamu vizuri tangu wakiwa na klabu ya AS Vita
Ni wazi Club Africain leo watakuja na mkakati wa kumdhibiti Mayele kwa kuwa ndiye mchezaji wanayemuhofia zaidi
Hata hivyo Mayele ni aina ya washambulliaji ambao akiwa katika ubora wake ni ngumu kumzuia
Lakini pia kama walinzi wa Club Africain watakuwa 'busy' kumzuia Mayele, inaweza kutoa mwanya kwa wachezaji wengine kufunga

Bernard Morrison, Stephane Aziz Ki na Feisal Salum kama watakuwa katika ubora wao siku ya leo, wanaweza kuiadhibu Club Africain
Yanga inahitaji kuwa na ufanisi mkubwa katika lango la Club Africain kuhakikisha wanatumia vyema nafasi wanazotengeneza