Jana baada ya kuwasili kutoka Sudan mshambuliaji wa Yanga Fiston Mayele alikiri kuwa wamewaangusha mashabiki wao kwa kushindwa kutua hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika
Ni baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Al Hilal kwa kufungwa bao 1-0 na kuondoshwa kwenye michuano hiyo kwa jumla ya mabao 2-1 katika michezo yote miwili
Mayele alisema yalikuwa matokeo magumu sana kwao lakini wanafahamu ni kwa kiasi gani mashabiki wao wameumizwa na matokeo hayo
Mayele alibainisha kuwa wachezaji walifanya kikao na kukubaliana mambo kadhaa ambayo wanapaswa kuyafanya ili kurejesha furaha ya mashabiki wao
"Baada ya mchezo kule Sudan wachezaji tulikaa kikao na kukubaliana mambo mawili. Kwanza tusahau matokeo ya ligi ya mabingwa na pili tujipange kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye kombe la Shirikisho"
"Tulipaswa kufanya vizuri kwenye mchezo dhidi ya Al Hilal lakini tulikosea katika mchezo wa kwanza baada ya kulazimishwa sare nyumbani"
Yanga leo inarejea mazoezi kuanza maandalizi ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba ambao utapigwa Jumapili, Oktoba 23 uwanja wa Benjamin Mkapa
Aidha siku ya leo pia Yanga itamfahamu mpinzani wake katika mchezo wa mtoano kombe la Shirikisho ambapo mchezo wa kwanza utapigwa Novemba 02 jijini Dar es salaam na marudiano kupigwa Novemba 09 ugenini